Monday, 9 April 2012

Uandishi wa Pendekezo la UtafitiPENDEKEZO LA UTAFITI

ANWANI YA UTAFITI
Uchanganuzi wa athari ya matumizi ya mafumbo katika kuwasilisha ujumbe wa mapenzi miongoni mwa wanafunzi wa chuo kikuu cha Maseno.

USULI
Kutokana na uchunguzi unaofanywa mara kwa mara na wataalam wa maswala ya mahaba na mahusiano wayaingiayo wanafunzi wa chuoni , ni bayana kuwa hali hii imesambaa na kugubika  jumuiya nzima ya vijana. Ili kijana yeyote ahisi kuwa ana sehemu katika jumuiya ya vijana wenzake, aghalabu huishia kujiingiza katika mahaba kwa jino na ukucha. Taasisi za kielimu hususan ndizo ambazo zimegeuka lindi la mapenzi. Baadhi ya vijana hufaulu ilhali wengine huambulia patupu. Kufua dafu kwao na kukosa kwao kwa asilimia kubwa hutegemea mawasiliano tofauti na sababu nyinginezo. Mawasiliano pia kwa upande wake hutegemea lugha kama chombo chake cha kufinyanga na kuwasilisha mawazo, hisia, na maelezo kwa njia na utaratibu fulani. Mwasilishaji wa ujumbe anaweza kutumia maneno, dhana au mitindo ya lugha ili kuafikia malengo yake.
Mipango mingi imezinduliwa nchini Kenya na watu binafsi, mashirika, dini mbalimbali ili kuwapa vijana mbinu na maneno watakayotumia katika kuwasilisha ujumbe wa mapenzi kwa mahabubu wao. Kwa ajili hii, matangazo yamekuwa yakienezwa kwenye vyombo vya habari mathalan magazeti, majarida, redio, runinga na zaidi katika mtandao, zikiwaeleza vijana kuulizia mistari watakayotumia kumtoa “nyoka pangoni.” Aghalabu, mistari hii huchukua mtindo wa kimafumbo ili kuonyesha uelewa wa lugha wa mwasilishaji na namna anavyomthamini mpenziwe.
Licha ya hayo, hata hivyo umefika wakati ambapo imekuwa muhimu kuelewa vijana, mawazo yao kuhusu mambo ya mapenzi na uwezo wao wa kudumisha mapenzi kwa kutumia mawasiliano ili kutafuta mbinu za kuwasaidia katika hawamu hii ya maisha ambayo huwa tatanishi kwa kijana yeyote.
Mafumbo ni sehemu mojawapo ya lugha ya Kiswahili ambayo hutumiwa katika kuwasilisha maana fiche. Kwa mujibu wa Wamitila K. L (2004), mafumbo hutumiwa kuelezea kauli ambazo huficha maana fulani au huweza kuwa maelezo marefu yaliyofumba kitu(au jibu) ambacho msikilizaji anaweza kukifumbua au kukielewa. Aidha, mafumbo haya yamegawika katika vipera vitatu vikuu: vitendawili, chemshabongo, mafumbo na mizungu.
Mapenzi ni kama chakula. Matumizi ya mafumbo ni kiungo muhimu na maalum ya kuongeza ladha kwa njia ya mawasiliano.
Vijana ambao hawajaasi ukapera huchumbiana kwa wingi kwa madhumuni ya kumpata ambaye atakuwa wake wa ubani. Kwa hivyo, nimeonelea kuwa ni muhali kwangu kuchunguza ili kuelewa ikiwa wao hutumia lugha fiche katika kuwasiliana. Nitakayorejelea ni mahaba yaliyopo baina ya vijana wa kiume na wa kike kwa sababu ulimwengu wa sasa umeshuhudia mapenzi ya jinsia moja! Nitashughulikia tu mapenzi baina ya jinsia ya kike na kiume.
 Kiini kikuu hasa cha kufahamu sehemu hii ya maisha ni kwa kutazama namna mawasiliano yao hufanyika. Na mawasiliano haya hutegemea lugha, maana na sanaa katika mawasiliano. Nadharia nitakazotumia kumulika suala hili ni pamoja na nadharia ya Ubunilizi, Mguso na Umaanishaji.
Mafumbo husaidia kutia utamu katika mawasiliano baina ya wapendanao iwapo yatatumiwa vyema.
Kwa hivyo, nitataka kuchunguza iwapo mtindo huu wa kimafumbo umeboresha au kujenga mahusiano ya mahaba miongoni mwa vijana (wa kike na kiume) katika Chuo Kikuu cha Maseno.   Kutokana na mambo haya yote,utafiti huu unalenga kukusanya data itakayoniwezesha kuratibu, kuchanganua na kuwasilisha matokeo ya athari ya matumizi ya mafumbo ya Kiswahili katika kufinyanga ujumbe ili kujenga  mapenzi miongoni mwa vijana wa Chuo Kikuu cha Maseno. 

SUALA LA UTAFITI
Mafumbo katika lugha yoyote ile huwa yana sehemu yake na umuhimu wake katika kufanya mawasiliano yaliyo fiche na yenye utajiri fulani unaokusudiwa na mwasilishaji wa ujumbe. Matumizi  yake yameathiri kwa njia moja ama nyingine namna wapendanao wanavyoonyeshana mahaba. Athari hizi zaweza kuwa chanya au hasi kutegemea :
·         Mazingira ya mawasiliano
·         Madhumuni ya ujumbe husika
·         Hekima ya utafsiri alio nao mlengwa wa ujumbe
·         Kiwango cha uhusiano au uchumba
·         Uthamini unaowekewa uhusiano wenyewe, miongoni mwa nyingine nyingi
Iwapo vipengele hivi havitazingatiwa na wapenzi wowote wale, kuna uwezekano mkubwa kuwa kutatokea mgongano wa kimawasiliano tofauti na endapo vitazingatiwa ambapo huleta mwingiliano, mwelewano na hivyo kuboresha mahaba.
Kutokana na hili, utafiti huu utasaidia kutathmini jinsi lugha ya mafumbo huchangia kujenga mawasiliano baina ya wapenzi hususan miongoni mwa vijana katika Chuo Kikuu cha Maseno.

MADHUMUNI YA UTAFITI 
Katika utafiti huu, ninalenga kukusanya data nitakayochanganua na hatimaye kuwasilisha kutokana na maoni nitakayopata kutoka kwa kundi wakilishi au sampuli ninayotafitia. Utafiti huu una malengo katika sehemu mbili; ya jumla na yale mahususi.
Malengo ya Jumla
·         Kufahamisha vijana kuhusu ubora wa kutumia lugha ya mafumbo katika kutia utamu mahaba yao
·         Kuelimisha vijana waelewe athari mbaya itokanayo na kutotumia lugha ya mafumbo ipasavyo
Malengo Mahususi
·         Kubaini namna kundi wakilishi linavyotumia lugha ya mafumbo katika mahaba
·         Kuonyesha faida ya mafumbo katika mawasiliana baina ya wapendanao
·         Kujua kina nani hasa hutumia lugha ya mafumbo katika kukamilisha mawasiliano ya uchumba katika kundi lengwa
·         Kutathmini ni mara ngapi kundi lengwa linatumia mtindo huu wa lugha katika mawasiliano
·         Utafiti huu pia hulenga kupima ni kwa kiwango kipi mafumbo yanayotumika huchangia kuibuka kwa misimu mipya
·         Kubashiri mtindo wa mapenzi baina ya vijana katika siku zijazo

MISINGI YA UTEUZI
Kuna sababu maalum ambazo zimenisukuma nifanye utafiti wangu katika Chuo Kikuu cha Maseno kwa wakati huu:

Mahali
Imekuwa muhali kutafitia swala hili katika Chuo cha Maseno kwa sababu, kwanza, ni karibu. Ukaribu huu utarahisha utafiti wenyewe kwa kuwa nitakuwa na muda wa kutosha ili kukusanya data ambazo hazitakuwa egemezi na za kuaminika. Maeneo mengine pia yanafaa kwa utafiti. Nilitambua kuwa swala hili halijatafitiwa katika chuo chenyewe na kwa hivyo, imefaa kufanyia Maseno.
Jambo la pili ni kuhusu rasilimali zilizoko. Kwa kutambua kuwa utafiti huu unahitaji fedha na muda ili kukamilisha na kuafikia malengo ya utafiti, hivyo basi, nikiufanyia utafiti wangu Chuoni Maseno ninaamini kuwa nitamudu gharama yenyewe pasi na uchechefu wowote ila yale yasiyokingika. Hii ni kwa sababu ninatazamia kutumia hojaji na njia ya mahojiano katika kukusanya data kutoka kwa kundi lengwa.

Wakati
Tofauti na kwamba nimechagua Chuo Kikuu cha Maseno kuwa uwanja wangu wa kutafitia, imenilazimu kufanya utafiti wangu kwa wakati huu kutokana na haja ya kutimiza masharti ya Kozi niifanyayo ili kufuzu na kupata shahada ya kiakademia.
Aidha, huu ni wakati ambapo wanafunzi wa kike hutungwa mimba. Kabla ya kufikia hatua hii, mahabubu hawa huwa wamechumbiana kwa muda fulani. Uchumba wenyewe hautakamilika na kufaulu ikiwa hakukuwa na mawasiliano yoyote. Kwa sababu hii, ninapania kuchunguza athari ya matumizi ya mafumbo katika mawasiliano yao ya kimapenzi.


Njia ya Utafiti
Katika kutafitia swala langu kikamilifu, ninanuia kutumia njia ya kihistoria kuwa njia ya kuendesha mchakato mzima wa utafiti.
Njia ya kihistoria itakuwa muhimu kwa kuwa nitakuwa nikichunguza mawasiliano baina ya wapenzi  tangu walipoanza kuchumbiana. Hii inamaana kuwa nitakuwa nikifuatilia mawasiliano yao kwa kipindi fulani kilichopita, ambayo ni historia.

Mbinu ya utafiti
Mbinu nitakayotumia katika kukusanya data itakayofanikisha utafiti mzima ni ile ya usaili na hojaji. Matumizi ya mbinu hizi mbili zitafaa ili niweze kufaidika na viziada (lugha ya kimwili) kando na yale atakayonielezea mlengwa katika kundi wakilishi.

Nadharia
Msingi wa utafiti huu kinadharia, utaegemea dhana ya Ubunilizi na ile ya Mguso pamoja na nadharia ya Umaanishaji. Kwa kuwa matumizi ya mafumbo katika mawasiliano huhusisha ubunifu kwa wanaotumia namna hiyo ya lugha, basi nadharia ya ubunilizi inayosisitiza kuwa mtunzi wa kazi ya fasihi ana uhuru wa kutunga mawazo yake ilimradi asikiuke kaida zilizowekwa.
Nadharia ya mguso kwa upande wa pili inaelezea kuwa kazi ya fasihi hulenga kwa njia moja ama nyingine mtu au watu kwa nia ya kuwaguza hadhira ili wafikirie sana kuhusus jambo lilowasilishwa na msimulizi.
Kando na hayo, nadharia ya Umaanishaji husisitiza maana katika mawasiliano ambayo kwa hakika, husaidiamtumiaji wa mafumbo kuzingatia mawasiliano kamilifu.
UPEO WA UTAFITI
Utafiti huu utashughulikia tu matumizi ya mafumbo kwa ujumla katika mawasiliano baina ya wapendanao. Isitoshe, itaegemea uhusiano wa kimapenzi kati ya kijana mvulana na kijana msichana.

NADHARIA
Kutokana na mada ninayotazamia kuchunguza, nimepata nadharia tatu zitakazoelekeza kazi hii. Mara kwa mara mapenzi ya kudumu huwa ni zao la ubunifu na nia walizo nazo wapenzi. Hapa huwa yahitaji lugha inayoweza kukamilisha “mradi” huu. Wale vijana ambao hujali kufaulu kwao katika mahaba ya dhati na ya kudumu, aghalabu huchukulia namna ya mawasiliano kuwa jambo nyeti.
Ili kujenga mawazo yangu kuhusu uchunguzi huu, nimepata nadharia ya Ubunilizi kuwa muhimu. Nadharia hii inashikilia kwamba yeyote ambaye ameingia katika jukwaa la utunzi, ana nafasi au uhuru wa kubuni mawazo yake na kuwasilisha kwa hadhira yake japo kwa upande mwingine, anahitajika kutilia maanani kaida zinazotawala maisha halisi ya jamii (Horace, 1975).
Nadharia yenyewe inazidi kuelezea kuwa kazi ya fasihi inahusu uwasilishaji wa maisha ya jamii kwa njia ya ubunifu na wala haigemei mambo ya kipekee.
Katika ubunifu wowote ule, huwa watunzi ambao wamejitosa hapa hutegemea kuwasilisha maana katika kazi yao ya kisanaa. Maana ama semantiki  huwa yajitokeza katika kazi zote za fasihi. Mtumiaji wa mafumbo kwa mara nyingi huwa anakabiliwa na jukuma la kuhakikisha kuwa mpokezi wa ujumbe wake anapata maana aliyoikusudia. Iwapo mafumbo atakayotumia hayatalingana kati ya wawasiliniaji, aghalabu huleta mgogoro ambao utaathiri uhusiano baina yao.
Kwa ujumla, matumizi ya mafumbo sharti yalenge kuwasilisha maana hata katika ubunifu wake.
 
Nadharia nyingine iliyo na uzito mkubwa katika utafiti huu ni nadharia ya mguso. Nadharia hii hutazama fasihi katika uhusiano wake na umma (hadhira) wake. Aidha, inaangazia mno kazi ya fasihi kwa hadhira. Hii inatokana na sababu kwamba kazi ya fasishi kwa njia moja ama nyingine, inalenga mtu au watu fulani.
Vasquez, A. S (1973:113) anasema kuwa kazi ya sanaa huathiri watu na inachangia katika kuhimiza au kupuuza dhana zao, maazimio yao, hata maadili yao. Anaamini kuwa ina msukumo wa kijamii ambao huathiri watu kwa nguvu zake za kihisia na kiititkadi. Anashikilia kuwa hakuna kwa hakika anayebaki vile vile baada ya ‘kuguswa’ na kazi halisi ya sanaa.
Nadharia hii inaelezea zaidi kuwa hadhira huishia kujitambulisha na wahusika kiasi cha kupoteza utambulisho wao wa asilia.
Wellek na Warren (1949:102) wanashuhudia kuwa watu wamewahi kubadilisha mienendo yao katika maisha kwa kuathiriwa na  wahusika wa kubuni katika fasihi.
Japo nadharia hii inakumbwa na changamoto ya kukadiria kiwango cha mguso, katika utafiti wangu natumai kuwa data nitakayokusanya zitaniwezesha kukabiliana na changamoto hii. Kwa sababu matumizi ya mafumbo ni kazi ya fasihi, natazamia kuwa kwa mujibu wa nadharia hii, kutakuwa na athari za wazi kati ya wapenzi wananotumia namna hiyo ya lugha.
Baadhi ya vijana siku siku hizi wanatumia mafumbo katika kuwasilishwa hisia zao za mapenzi kwa sababu mbalimbali ambazo utafiti huu pia utapambanua. Kwa hivyo, kazi hii ya kisanaa huwa una mguzo mkubwa mradi matumizi ya mafumbo yastahiki.   

Nadharia nyingine itakayofaa katika utafiti mzima ni ile ya Umaanishaji iliyoasisiwa na Grice (1975). Nadharia hii inaelezea kwamba kuwa watu huwa hawasemi mambo waziwazi; na ili kupata ujumbe kamilifu kutokana na kile wakisemacho, ni sharti kuwe na umaanishaji katika maana. Kauli hii imejengwa kwa msingi kuwa wasemaji humaanisha mambo yanayozidi walichokisema.
Kwa jumla, nadharia hii inashikilia dhana kuwa maana ya jambo, matukio au hali fulani hutokana na tafsiri ya kimuktadha pamoja na elimu shirikishi.  Yaani, maana ni zao la ushirikiano baina ya msikilizaji na msemaji kwa kuzingatia kaida nne: kanuni ya idadi, namna, uhusiano, na ukweli.
Kutokana na nadharia hii, ni wazi kuwa vijana wanaotumia mafumbo kama njia mojawapo ya kuwasilisha hisia zao kwa wapenzi wao, waangalie kuwa kanuni hizi zimezingatiwa ikiwa wanahitaji fanaki katika “mradi” wao. Mafumbo hukakanganya kimaana na hivyo basi itakuwa bora ikiwa ukweli na tafsiri bora inazingatiwa ili kupata maana halisi na kumtosheleza msikilizaji na msemaji.


MAPITIO YA MAANDISHI
Matumizi ya mafumbo huwasilisha maana japo si moja kwa moja kama ilivyo lugha ya wazi. Katika lugha ya wazi, mara nyingi mlengwa wa ujumbe hupata maana karibu mara moja ambayo ni tofauti na mafumbo ambayo huhitaji tafsiri ya maana ya hali ya juu. Kwa hivyo, kuwasilisha maana kwa kutumia lugha hii fiche, wapenzi wanajukumika kuhakikisha maana iliyokusudiwa ndiyo tu inayopokelewa. Kwa hivyo maana ni msingi katika kufinyanga ujumbe wa mapenzi.
Kwa mujibi wa Cruise (1986), maneno yanapofanyiwa uchunguzi wa kileksika, huibua aina nne za maana. Maana inaweza kuwa halisi(maana inayopatikana katika ulimwengu halisia au ubunifu wa mtunzi inayobainisha uwongo ama ukweli wa jambo linalozungumziwa), maana hisishi (maana inayojitokeza katika hisia husika; ambapo hufanya maneno mawili au zaidi yaliyo sawa kutofautiana kwa msingi wa hisia), maana husishi (maana ambayo huibuka kutegemea namna maneno yameungana kisarufi kulingana na vikwazo vya kimwandamano. Lengo lake ni kuleta maniyki katika usemi) na maana kimuktadha (ambayo ni maana inayoibuka kutegemea lahaja au sajili ambayo imetumika).
Katika matumizi ya mafumbo ya Kiswahili humaanisha mambo tofauti kwa vijana tofauti kutegemea elimu shirikishi iliyopo. Kwa hivyo, ili kujenga uhusiano wa kudumu, wapenzi sharti waangalie na kutathmini maana wanayowasilisha ili kuepuka migogoro na mizozo na kudumisha mapenzi yao.
Anderson (1987) anasema, “katika makundi yetu tofauti tunayoegemea, sote twapambana na dhana ya maana… dhana ya maana ni changamoto kwetu sote.” 
Anazidi kusema kuwa namna inavyofanya kazi, kufahamu na kuelezewa kwake ni jitihada ya pamoja.
Wasomi wengi wa mawasiliano hutazama mawasiliano kama mchakato-sifa, visababishi  na matokeo ya mawasiliano fulani yanategemea mabadiliko ya muda ya vitendo katika mawasiliano.
Kimuktadha, mchakato wa mawasiliano huwa imara kwa kuzingatia mahali na wakati wa utendaji wake.
Hata hivyo, mawasiliano hutusaidia ili tuweze kufahamu wenzetu tunaohusiana nao katika hali zao na mtazamo wao. Kwa hivyo, ili wapenzi wadumu katika mapenzi, mawasiliano ndicho chombo kama asemavyo Anderson.
”Mawasiliano ni muhimu katika kufahamu ulimwengu wetu. Lengo lake kuu ni mchakato wa maana” (Anderson 1987)
Kwa hili, maana inayowasilishwa kupitia mafumbo, kwa wakati mwingine hutofautiana ukizingatia mwasilishaji na mpokezi wa ujumbe.  Hii ni kwa sababu maana huwa katika nafsi ya mtu na hivyo inambidi mwasilishaji wa ujumbe kutafuta Kujua ikiwa maana ya kile alichowasilishwa imefika kwa namna na wakati aliokusudia. Na ikiwa haitakuwa hivyo, basi yafaa mwasilishaji kulainisha mambo kwa kubuni mbinu ya kurekebisha hali ili kusiwe na mgogoro wowote wa kimaana.
“Kwa mambo yote, mawasiliano ni la shani” ( Dewey, 1939:385)
 “Jamii haiishi tu kwa uwasilishaji, kwa mawasiliano, lakini inawezekana kusema pasi upendeleo kuwa huishi katika uwasilishaji, na mawasiliano.” (Dewey, 1916:3)
“Mawasiliano yanaanza katika jitihada za kujifunza na kuelezea. Ili kuanzisha mchakato huu katika mawazo yetu na kupitisha matokeo yake kwa wengine, twategemea vielelezo fulani vya mawasiliano, utaratibu fulani au maagano ambayo kwayo tunaweza kuwasiliana.” (Williams, 1966: 19-20).
“Akili zetu na maisha yetu yananatawaliwa na jumla ya tajriba zetu- au zaidi, kwa ishara za tajriba… na jina la tajriba yenyewe ni mawasiliano.”


UMUHIMU WA UTAFITI
Utafiti huu utalenga kuibua data ambayo inaweza kutumika na wachanganuzi wa maswala ya mahusiano na mlahaka kuelezea athari ya mawsiliano zinazotokana na matumizi ya lugha fiche.
Itawasaidia pia vijana kufahamu namna mtindo wa kutumia mafumbo katika mapenzi yao hufanikisha  au kuporomosha kutegemea namna wanavyotumia.   


NJIA NA MBINU ZA UTAFITI
Ili kukamilisha utafiti huu na kuibua data mpya kuhusu suala la utafiti, ninalenga kutumia njia ya kihistoria. Njia ya kihistoria inafaa katika utafiti huu kwa kuwa huwezesha kupata ukweli wa matukio ili kubashiri hali ya baadaye ya jamii pana ninayotafitia. Njia hii pia husaidia katika kuchunguza mtu binafsi. Aidha, hii ni njia ambapo mtafiti anaweza kufuatilia matukio yaliyopita ili kuelezea hali ilyopo.
Kwa ajili hii, itanibidi nichunguze namna wapenzi wamekuwa wakitumia mafumbo katika uhusiano wao tangu walipoanza kuchumbiana. Kwa hivyo, data zitakayopatikana zitategemea uwezo wa mlengwa wa kuhifadhi matukio yaliyopita.
Kwengineko, katika utafiti huu nitatumia mbinu mbili za utafiti ambazo ni ya hojaji na usaili.
Hojaji hii itajumuisha maswali funge tu na sehemu muhimu zitakazosaidia kuthibitisha au kupinga nadharia tete pamoja na kuafikia malengo ya utafiti wenyewe.
Usaili utakuwa muhimu pia ili kuninufaisha na viziada ligha(lugha ya mwili) ambavyo vitakuwa vigumu kushirikisha katika hojaji. Mbinu hii inalenga kupata ufafanuzi kutoka kwa walengwa kuhusu hoja muhimu ya hojaji ili kupata data zinazoakisi hali halisi ya mambo pasi kuegemea upande.  


NADHARIA TETE
Ikiwa matumizi ya mafumbo katika lugha yanahusiana na ujumbe uliowasilishwa, kwa hivyo basi, utumiaji wake katika mapenzi hudumisha uhusiano baina ya wapenzi vijana


UTEUZI WA SAMPULI
Ili kupata kundi wakilishi kutoka jamii pana ninayojishughulisha nayo, nitazingatia uteuzi sampuli wa mtabakisho katika hatua ya kwanza. Kufanya huku kutaniwezesha kupata vijisehemu vilipo kundi wakilishi. Kwa muktadha huu, vijisehemu hivi vitajumuisha idara na skuli zote za kiakademia zinazopatikana katika Chuo cha Maseno.
Hatua itakayofuatia katika uteuzi wa sampuli itakuwa uteuzi sampuli kimaksudi . Hatua hii itaniwezesha kupata walengwa binafsi ili kuwahoji. Kwa sababu ya wingi wao, nitateua tu walengwa sita kutoka kila idara na skuli huku nikizingatia usawa wa kijinsia ambapo nitateua walengwa watatu wa kike na watatu wa kume.MAREJELEO
Wamitila K. W. (2004). Kichocheo cha Fasihi Simulizi na Andishi. 2nd ed. Focus Publications Ltd, Enlish Press. Nairobi. Kenya.
 Anderson, J(1987). Communication Research Issues and Methods. ISBN 0-07-001 651-8. McGraw Hill.
 Carey, J. W(1992). Communication as Culture, Essays on Media and Society. 2nd ed. New York, London.
Enlish, J. et al (2006). Professional Communication, How to Deliver Effective Written and Spoken Messages. 2nd ed. Juta & Co. Ltd. Lansdowne 7779.   
Ntarangwi, M. (2004). Augustane College, Rock Island, IL 61201
Grice H. P (1975). Implicator Theory.
National Health Museum. Writing Hypothesis.